Shirika La Afya Duniani Kuamua Kuhusu Chanjo Za Covid-19 Za China
Shirika La Afya Duniani Kuamua Kuhusu Chanjo Za Covid-19 Za China

Shirika la Afya Duniani, WHO baadae wiki hii litaamua iwapo liidhinishe chanjo mbili za China kwa matumizi ya dharura dhidi ya ugonjwa wa COVID-19. 

Iwapo zitaidhinishwa zitakuwa chanjo za kwanza kutoka China na kuwekwa katika orodha ya matumizi ya dharura ya shirika hilo. 

Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa WHO, Mariangela Simao anayehusika na upatikanaji wa dawa na chanjo, amesema wanatarajia kwamba maamuzi yote yatatolewa mwishoni mwa wiki hii. 

WHO imesema inatarajia uamuzi wa chanjo ya Sinopharm kuanza kutumika kwanza kabla ya Sinovac. 

Wakati huo huo, Umoja wa Ulaya umeanza kupeleka chanjo za virusi vya corona zilizofadhiliwa na umoja huo kwenye nchi za ukanda wa Balkan, ambako China na Urusi kwa miezi kadhaa zimekuwa zikipeleka chanjo hizo zinazohitajika. 

Mwezi uliopita Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya ilitangaza itapeleka dozi 651,000 za Pfizer nchini Serbia, Bosnia, Macedonia Kaskazini, Montenegro, Albania na Kosovo.