Mkutano Wa G7 Wamalizika Kwa Kukemea China, Urusi, Iran
Mkutano Wa G7 Wamalizika Kwa Kukemea China, Urusi, Iran

Kundi la nchi saba tajiri ulimwenguni limekamilisha mkutano wake wa kwanza wa ana kwa ana katika zaidi ya miaka miwili, likiishutumu China kwa ukiukaji wa haki za binaadamu na ukandamizaji dhidi ya wapigania demokrasia.


Mawaziri wa mambo ya kigeni kutoka taifa mwenyeji Uingereza, pamoja na Marekani, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Canada na Japan pia wametoa wito kwa Iran kuwaachia huru raia wa kigeni na walio na uraia wa nchi mbili waliosema kuwa wanazuiliwa kiholela katika magereza ya Iran.

Wametishia kuliwekea vikwazo vipya jeshi la Myanmar ambalo lilifanya mapinduzi Februari mosi. 

Walijadili pia masuala ya mabadiliko ya tabia nchi na jinsi ya kujikwamua baada ya janga la corona.

Mataifa hayo yameahidi msaada wa kifedha kwa mpango wa kugawana chanjo wa Covax. Kundi hilo tayari limeahidi Zaidi ya dola bilioni 10.7.

Lakini hakukuwa na tangazo la haraka kuhusu ufadhili mpya wa kuimarisha upatikanaji mkubwa wa chanjo, licha ya miito inayorudiwa kwa G7 kuongeza juhudi za kuzisaidia nchi maskini.

Watetezi wa haki walilitaka Kundi la G7 kuimarisha juhudi za kupambana na ukosefu wa usawa katika vita dhidi ya janga la corona, wakati nchi za Magharibi zikizidisha kampeni zao za utoaji chanjo na kufungua shughuli za kiuchumi.