Mamlaka ya Dawa ya Marekani inajiandaa kuidhinisha mapema wiki ijayo chanjo dhidi ya Corona iliyotengenezwa na maabara ya Pfizer na BioNTech kwa vijana wenye umri wa miaka 12 hadi 15, Gazeti la New York Times limeripoti, likinukuu maafisa wa shirikisho katika mchakato huo.
Idhini katika mwelekeo huu kutoka kwa FDA (Mamlaka ya Chakula na Dawa) ilitarajiwa tangu Maabara ya Marekani na Ujerumani zilipotangaza mwezi Machi kwamba majaribio ya kliniki yameonyesha kuwa chanjo yao iko salama, yenye ufanisi na inazalisha kingamwili zenye nguvu kwa vijana wenye umri wa miaka 12- 15.
Wakati huo huo FDA imesema inachunguza uwezekano wa kupanua idhini ya chanjo, bila kutoa maelezo zaidi.
Chanjo ya COVID-19 iliyotengenezwa na maabara ya Pfizer-BioNTech tayari imeruhusiwa nchini Marekani kwa watu walio na umri zaidi ya miaka 16.
Maabara ya Moderna na Johnson & Johnson pia wanajaribu chanjo zao kwa vijana. Takwimu kutoka kwa majaribio ya kliniki yaliyofanywa na maabara ya Moderna zinatarajiwa kutolewa hivi karibuni.